Kwa mujibu wa ripota wa Idara ya Kimataifa ya Shirika la Habari la Hawza, Dkt. Manal Fanjan, mhadhiri wa Sheria za Kimataifa katika chuo kikuu nchini Iraq, katika kikao cha saba cha kimataifa cha “Mwamko Mpya wa Umma wa Muhammad (saww)”, kilichofanyika Jumatano, kwa juhudi za Jumuiya ya Kimataifa ya Qadimun, akizungumzia maendeleo ya kikanda na makabiliano ya Iran dhidi ya Marekani na utawala wa Kizayuni, alisisitiza umuhimu wa Umma wa Kiislamu kutumia mazingira ya sasa ili kufafanua upya nafasi yake katika mizania ya mahusiano ya kimataifa.
Akieleza kwamba ulimwengu wa Kiislamu uko katika hatua nyeti na ya kuamua mustakabali wa historia yake, alisema: Mipango iliyowasilishwa tangu miaka ya 1970 kwa jina la “Mashariki ya Kati Mpya”, na baadaye kupanuliwa sura ya wazo la “Mashariki ya Kati Kubwa”, ililenga kubadilisha mizania ya nguvu katika eneo hili na kuimarisha ubora na utawala wa utawala wa Kizayuni.
Kwa mujibu wa maelezo yake, maendeleo yanayohusu Palestina, Lebanon, Yemen, Iran na Iraq yanapaswa kuchambuliwa ndani ya mfumo wa mipango hiyo na juhudi za kuweka utawala na mamlaka juu ya nchi za eneo hili.
Fanjan aliongeza: Ingawa Iran, katika hali ya sasa, inakabiliwa moja kwa moja na mashinikizo na mashambulizi ya kijeshi, na imelipa gharama kubwa, matokeo ya maendeleo haya hayatabaki katika mipaka ya nchi moja pekee. Bali, nchi zote za eneo hili, hata zile zinazodhani kuwa ziko mbali na mwenendo huu au zinazoshirikiana nao, zinaweza kuathiriwa. Kwa hiyo, mataifa na Serikali za Kiislamu zinapaswa kuchunguza kwa utambuzi na mtazamo wa mbali zaidi hali halisi iliyojificha nyuma ya maendeleo haya.
Akizungumzia uwezekano wa kuyageuza machafuko na migogoro kuwa fursa, alitaja mambo sita yanayoweza kusaidia kunufaika na mazingira magumu: kushikamana na njia na msingi ulio wazi; umoja unaojengwa juu ya misingi ya pamoja; uimara na kutoyumba; subira; kuimarisha uwezo wa ulinzi; na kumtegemea Mwenyezi Mungu. Kwa kurejelea aya isemayo:
الَّذِينَ قَالَ لَهُمُ النَّاسُ إِنَّ النَّاسَ قَدْ جَمَعُوا لَكُمْ فَاخْشَوْهُمْ فَزَادَهُمْ إِيمَانًا وَقَالُوا حَسْبُنَا اللَّهُ وَنِعْمَ الْوَكِيلُ
“Wale ambao watu waliwaambia: ‘Hakika watu wamekusanyikeni kwa ajili ya kukushambulieni, basi waogopeni.’ Lakini jambo hilo likawazidishia imani, nao wakasema: ‘Mwenyezi Mungu anatutosha, naye ni Mbora wa Mtegemewa.’”
Alisisitiza kwamba, katika kukabiliana na vitisho, kuhifadhi imani na azma ya pamoja kuna umuhimu wa msingi.
Mhadhiri huyo wa Sheria za Kimataifa nchini Iraq, akizungumzia muqawama wa wananchi na Serikali ya Iran mbele ya mashinikizo ya kijeshi na kiuchumi, aliutaja uimara huo kuwa ni fursa ya kuimarisha mshikamano wa ulimwengu wa Kiislamu, na kusema: Nchi za Kiislamu zinapaswa kunufaika na uzoefu huu ili kuongeza nafasi yao katika mizania ya nguvu duniani, na zisiiruhusu tofauti za ndani kudhoofisha uwezo na rasilimali za Umma wa Kiislamu.
Aidha, alisisitiza umuhimu wa kuanzishwa mfumo wa pamoja wa kiusalama na kiulinzi baina ya nchi za Kiislamu, na kuzitaja Uturuki, Iran, Iraq, Saudi Arabia na Misri kuwa ni miongoni mwa nchi zinazoweza kuwa na nafasi katika kuunda mfumo wa aina hiyo. Kwa mujibu wa maelezo yake, ushirikiano wa kiulinzi wa kikanda unaweza kuweka mazingira ya kupunguza utegemezi wa kiusalama kwa madola ya kigeni na kuongeza uwezo wa nchi za Kiislamu katika kulinda maslahi yao, rasilimali zao za kiuchumi na utajiri wao.
Katika kuendelea na maelezo yake, Fanjan, akizungumzia ziara za ujumbe kutoka Uturuki, Pakistan na Saudi Arabia nchini Iran, alielezea matumaini yake kwamba mashauriano ya aina hiyo yatafanyika kwa msingi wa utashi huru wa nchi za Kiislamu na kwa lengo la kuimarisha ushirikiano baina yao.
Mwisho, alisisitiza kwamba: Mwamko mpya wa Umma wa Muhammad (saww) utatimia pale Waislamu watakapoweza kuvuka hali ya sasa kwa njia ya umoja, kushikamana na Uislamu, kuchukua msimamo ulio wazi na kuimarisha uwezo wao wa ulinzi, na hatimaye kuwa nguvu yenye ushawishi katika mizania ya mahusiano ya kimataifa.
Dkt. Manal Fanjan alihitimisha hotuba yake kwa dua ya kuiombea Iran, Palestina, Lebanon, Yemen, Iraq na nchi nyingine za Kiislamu ushindi na usalama, pamoja na kuelezea matumaini yake ya kuundwa mfumo mpya wa kikanda unaojengwa juu ya heshima, uhuru na kulinda maslahi ya mataifa ya Kiislamu.
Maoni yako